Lugha na Utandawazi
Nafasi ya Kiswahili katika Kukuza na Kuendeleza Demokrasia nchini Kenya
Keywords:
Utandawazi, Lugha, Demokrasia, MaendeleoAbstract
Lugha huwa na nafasi kubwa katika maisha ya jamii huku mawasiliano yakiwa mojawapo wa majukumu yake. Awali, jamii mbalimbali zilikuwa zikijichukulia kama kwamba zimejitenga na jamii nyingine zikiwa na jinsi ya kufanya shughuli zao kivyao. Hii leo, utandawazi umekita na kila jambo linatazamwa kwa muktadha wa dunia kuwa kijiji. Demokrasia ni falsafa ya kisiasa inayoenea kote duniani kwa haraka. Kwa misingi hii, falsafa inatakiwa kuchanganuliwa kwa mujibu wa taaluma zingine za utamaduni kama vile lugha. Kwa hivyo, makala hii inanuia kubainisha nafasi ya lugha katika kukuza demokrasia na uongozi mwema. Inapendekeza matumizi ya Kiswahili na lugha za kiasili kama nyenzo za kukuza na kueneza demokrasia katika muktadha wa bara la Afrika. Pia, inaangazia jinsi taasisi za kijamiii kama katiba, mahakama, tume za uchaguzi, vyombo vya habari na makundi ya kutetea haki za kijamii yanavyotumia Kiswahili kutetea na kuendeleza demokrasia. Inatazamiwa kwamba makala hii itachangia upanuzi wa maarifa katika taaluma ya isimu-jamii, hasa nyanja za uongozi na utawala na majukumu ya lugha. Hatimaye makala hii inapendekeza kwamba lugha ya Kiswahili itumike kufundisha somo la mawasiliano katika ngazi ya chuo kikuu ili kutilia nguvu matumizi yake na wataalamu wanaohitimu katika nyanja mbalimbali.