Mchango wa Mbinu ya Familia Wenyeji katika Ufundishaji na Ujifunzaji Darasani wa Kiswahili kama Lugha ya Kigeni
Keywords:
Mbinu, Familia, Wenyeji, Ujifunzaji, UfundishajiAbstract
Familia Wenyeji ni moja kati ya mbinu mashuhuri zinazotumika katika ufundishaji wa lugha za kigeni kwa kuzingatia ufundishaji kimawasiliano. Tafiti mbalimbali zimeonesha umuhimu na ufaafu wa mbinu hii katika maendeleo ya ujifunzaji lugha kwa wajifunzaji wa lugha ya kigeni. Licha ya kuwepo uhusiano kati ya mbinu hii na ufundishaji na ujifunzaji wa lugha darasani, tafiti hizo hazikuonesha mchango wa matumizi ya mbinu hiyo katika ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya kigeni darasani. Makala hii imebainisha mchango wa mbinu hiyo katika ufundishaji na ujifunzaji wa darasani wa Kiswahili kama lugha ya kigeni kwa kuchunguza ni kwa namna gani walimu na wajifunzaji wanatumia familia wenyeji kama mbinu ya kufanikisha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji wa darasani. Data za makala hii zimetokana na mahojiano yaliyofanyika kwa kuhusisha walimu wa Kiswahili kwa wageni, wajifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni na waratibu wa familia wenyeji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar na Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC) na kuchambuliwa kwa mkabala wa kimaelezo na kuongozwa na Nadharia ya Umahiri wa Kimawasiliano na Tamaduni Mchanganyiko ya Hall (1992). Matokeo ya utafiti yaliyojadiliwa katika makala hii yameonesha upo mchango wa matumizi ya mbinu hii katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni darasani.