Mwachano wa Taratibu za Uundaji wa Istilahi za Kiswahili na Changamoto Zake katika Lugha

Mifano kutoka Istilahi za TATAKI na BAKITA

Authors

  • Joseph Isindikiro Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Author

Keywords:

Istilahi, Dhana, Taratibu, Hatua, Mwongozo, Mchakato, Jopo

Abstract

Suala la uundaji wa istilahi katika lugha limekuwa ni la muda mrefu, hivyo, linapaswa kuratibiwa kwa taratibu maalumu na za kudumu. Taratibu hizo zinapaswa kuwa bayana na zisizobadilika jambo linalotajwa kuchochea kudumishwa kwa nidhamu katika mchakato wa uundaji wa istilahi. Utafiti ulilenga kuchunguza mabadiliko katika taratibu mbalimbali za uundaji wa istilahi za lugha ya Kiswahili na changamoto zake katika istilahi zinazoundwa katika mazingira hayo. Taratibu zilihusisha: hatua za uundaji wa istilahi, miongozo inayotumika na ushirikishwaji wa wataalamu wa istilahi kutoka nchi nyingine zinazotumia lugha ya Kiswahili.  Data za utafiti zilikusanywa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, BAKITA na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine. Mbinu ya usomaji nyaraka maktabani, hojaji na usaili zilitumika kupata data. Data zilikusanywa kwa kuongozwa na nadharia ya Jumla ya Istilahi na kujalizwa na nadharia ya Istilahi za Kisayansi na kuchanganuliwa kwa mkabala wa kitaamuli. Matokeo yamebainishwa kuwa; kila jopo lina hatua zinazofuatwa jambo linaloweza kuchochea kuundwa kwa istilahi zenye changamoto katika lugha. Pia matokeo yamebainishwa kuwa licha ya mwongozo wa BAKITA kuonekana una manufaa zaidi katika kuunda istilahi za Kiswahili, bado pamekuwa na matumizi ya kuchanganya miongozo. Matokeo yameeleza changamoto na mabadiliko yanayoukumba msisitizo unaotolewa na mwongozo wa ISO, hivyo, kuufanya ushindwe kutekelezeka kikamilifu. Kuhusu ushirikishwaji wa wataalamu wa lugha ya Kiswahili kutoka nchi nyingine, imebainishwa kuwa ushirikishwaji umekuwa ukifanyika kwa kiwango kidogo na mara nyingine, nchi zinazoshirikishwa hubadilika takribani kila jopo. Matokeo yamehimiza haja ya kuwa na utaratibu maalumu, bayana na pangilifu katika kuunda istilahi za lugha. Pia, matokeo yamehimiza kuwapo kwa juhudi za pamoja za nchi watumiaji wa Kiswahili ili kukipa Kiswahili sura moja katika eneo lote kinamotumika na kuipunguzia lugha mzigo wa istilahi zenye sura ya kanda.

Downloads

Published

30-04-2023

Issue

Section

Articles