Tafsiri Tenge katika Matini Zilizotafsiriwa kwa Tafsiri-Mashine
Uchanganuzi wa Matini za Kiingereza-Kiswahili
Keywords:
Tafsiri tenge, Tafsiri-Mashine, lugha chanzi, lugha lengwa, matiniAbstract
Makala haya yanachunguza mchakato wa kutafsiri kwa Tafsiri-Mashine. Tafsiri- Mashine baina ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza hutumiwa na wasomi, wafasiri, watalii, watafiti na wajifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni au ya pili. Kwa hivyo, ni nyenzo muhimu katika mchakato wa kutafsiri matini. Hata hivyo, mchakato huu unakabiliwa na changamoto za tafsiri tenge kama inavyodhihirika katika makala haya. Mbinu ya uchambuzi wa matiniilitumiwa kukusanya data iliyojenga msingi wa makala haya. Matini zilizotafsiriwa kwa kutumia Tafsiri- Mashine (kuanzia sasa, TM) zilichanganuliwa kiulinganishi. Matokeo yanaonesha kwamba tafsiri ya neno kwa neno inayotumika kwa upana katika TM ina upungufu katika kuhawilisha maana kutoka Kiingereza (lugha chanzi) kwenda Kiswahili (lugha lengwa). Tafsiri haihusishi tu maneno na sentensi bali ni mchakato changamani unaohusisha vipengele vingi. Mwandishi wa makala haya ameonesha mifano anuwai ya tafsiri tenge na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo. Matokeo ya utafiti huu yamebainisha kwamba lugha nyingi za Kiafrika ikiwemo lugha ya Kiswahili, hazijaweza kufaidi katika mbinu hii ya kutafsiri kwa mashine (kompyuta).